DHANA YA MPANGO WA UHAMASISHAJI NA
UKUSANYAJI WA RASILIMALI 2018-2020
"Tuwawezeshe kwa Rasilimali zetu"
Kwa miongo Zaidi ya mitatu
idadi ya vijana nchini Tanzania imekuwa ni Zaidi ya asilimila 60, na hivyo
kufanya idadi ya vijana kuonekana kubwa Zaidi ya kundi lolote la kijamii, yaani
wazee, wanawake, na watoto. Idadi hiyo inaonekana kwenye maeneo yote ya mijini
na vijijini, na hivyo kufanya wadau mbalimbali ikiwemo serikali kuhakikisha
kundi hili linapewa kipaumbele kwenye maswala yote ya maendeleo ikiwemo uchumi,
afya, siasa, utamaduni na maswala ya kijamii. Jitihada za serikali kwa muda
mrefu zimekuwa zikilenga kuona vijana wote wanatumika kikamilifu kwa uzalishaji
na kuleta tija kwa taifa kupitia uongozi, maswala ya kilimo, Afya na kukuza
teknolojia.
Zimekuwepo kauli mbiu
na vibwagizo mbalimbali vya kuhamasisha utayari wa vijana kuwajibika na
kutumikia taifa kiuzalendo, vibwagizo kama “Vijana ni nguvu kazi ya taifa”,
“Vijana ni taifa la leo” hizi zote zimekuwa zikilenga kuwaandaa vijana
kujitambua na kuchukua nafasi yao kama kundi muhimu linalotegemewa na taifa
kwenye Nyanja zote za maisha ikiwemo ulinzi na usalama wa taifa letu.
Pamoja na jitihada
zote, ikiwemo upatikanaji wa sera ya maendeleo ya vijana na mipango mikakati
mbalimbali ya vijana na biashara, vijana na utamaduni, vijana na ushiriki
kwenye kilimo; bado kumekuwepo na changamoto kubwa hususani kwenye upatikanaji
wa ajira kutoka serikalini na sekta binafsi na ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kujiajiri.
Kama zilivyo nchi
nyingi barani Afrika, Tanzania pia ni nchi yenye asilimia kubwa ya vijana
wasiokuwa na kazi rasmi, na wengi wa vijana hao wanapatika vijijini. Ni miaka
ya hivi karibuni ya 2000, nchi yetu imeshuhudia umbwe kubwa la vijana wakihama
kutoka vijijini na kuhamia mijini kutafuta ajira na huduma nzuri za kijamii.
Kwa upande mwingine ukosefu wa ajira kwa vijana umepelekea mchango wa vijana
kwenye taifa lao kuwa mdogo na wengine kutokuwa na mchango kabisa kwenye ujenzi
wa Taifa. Ni mara nyingi na kwenye maeneo mengi ya Tanzania, Mikoani na
wilayani, Mjini na Vijijini tunashuhudia
vijana wengi wakijihusisha na matendo ya hatari kama uzururaji, uvutaji
wa bangi, sigara na madawa ya kulevya, wizi, ujambazi wa kutumia silaha,
umalaya na ukatili; haya yote yamepelekea vijana kutoaminiwa na kutoshirikishwa
kwenye shughuli na masuala mengi ya kijamii na kitaifa. Mfano, ushiriki wa
vijana kwenye mipango na mgawanyo wa rasilimali za maeneo yao (Mitaa, kata,
wilaya, Mkoa na Taifa). Hali hii imewanyima uwakilishi wenye tija na unaofuata
mtiririko kwenye maeneo na ngazi mbalimbali za serikali.
Tukiwa tunashuhudia
matendo ya hatari kwa vijana waliowengi nchini, bado tunasikia jamii inalia juu
ya maadili duni na ya kutilia shaka juu ya Mavazi, Lugha, na matendo yasiyokuwa
na dhamiri iliyohai. Door of Hope to
Women and Youth Tanzania (DHWYT), imejizatiti na imejipanga kuendelea na
program mbalimbali za kuwawezesha na kuwasaidia vijana kwenye nyanja zote za
kiuchumi, Kijamii, Kitamaduni, kisera, na kimfumo. DHWYT siku zote tumeweza kufanya haya yote kwa mafanikio kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali wa vijana kutoka ndani na nje ya nchi, Serikali ya Tanzania
ikiwa ni mdau namba moja. Mbinu ya Utetezi zinatumika kutatua changamoto zote
za vijana za kimfumo na kisera, na kwenye changamoto za uelewa(haki
na wajibu) na hamasa kwa vijana, mbinu za Mafunzo ya kujengeana uwezo,
Makongamano, mikutano, midahalo na uundaji wa vikundi vya vijana wenye mlengo
mmoja zitatumika. Programu kama “Elimu ya Uraia, ufuatiliaji wa uwajibikaji
kwa jamii”, “Uimarishaji wa Uchumi na Ujasiriamali”,
“Vijana
na Maadili ya Jamii ya Kitanzania” pamoja na programu ya “Vijana
na Mawasiliano” zimeendelea kutolewa na shirika. DHWYT kama taasisi ya
kuwezesha vijana na wanawake nchini Tanzania itatekeleza programu hizi nchi
nzima.
DHWYT
ni shirika lisilokuwa la kiserikali lililojipambanua na kujizatiti kufanya kazi
ya kusaidia na kuwezesha vijana na wanawake nchini Tanzania. DHWYT limesajiliwa
kwa mujibu wa sheria namba 24, ya 2002, na nambari ya usajasili ni
00NGO/0009273; na hivyo kupewa mamlaka ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya
vijana na wanawake Tanzania bara. Hadi sasa shirika limeweza kuimarisha
shughuli za uwezeshaji kwenye wilaya saba ndani ya mikoa ya Lindi, Mtwara,
Kagera na Kigoma, na lengo ni kufikia Mikoa yote ya Tanzania bara.
Lengo kuu la taasisi,
ni Kuwa na Vijana na Wanawake waliowezeshwa wenye uwezo wa kutumia akili na
nguvu zao, kubaini na kutumia fursa za kitaifa kwa ajili ya maendeleo endelevu
ya kijamii na kiuchumi.
Shirika la DHWYT mpaka
sasa limeweza kuwafikia vijana na wanawake kupitia programu za *Uwezeshaji wa
kiuchumi na ujasiriamali *Ufuatilianji wa Uwajibikaji kwa jamii *Elimu ya Uraia
*Afya, Unasihi wa Lishe na Huduma, pamoja na *Utawala bora kwenye tasnia ya
uziduaji –gesi, mafuta na madini.
Katika kufanikisha ufikiwaji wa vijana wengi, shirika limekuwa likitumia njia ya
kukusanya rasilimali kutoka nje na ndani ya nchi, kwa kuwafikia sekta binafsi,mashirika
ya umma, wadau wa maendeleo, vijana na wanawake kuchangia mahitaji na bajeti
kubwa ya taasisi.
Tokea uwanzishwaji wa
mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na Asasi za kiraia nchini tanzania
pamekuwepo na utegemezi wa misaada na ruzuku za uwanzishwaji, uimarishaji na
uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa makundi yote ya kijamii, hasa
watoto,vijana na wanawake kutoka kwa wadau wa maendeleo wa nje ya Tanzania
(Wafadhili na Wabia). Kwa mazingira hayo utelekezaji wa shughuli za uwezeshaji,
utetezi na huduma zinategemea hali ya kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia kwenye
nchi husika. Mpaka sasa asilimia 97 ya pesa zinazoendesha miradi ya maendeleo
kwenye programu na miradi ya utetezi, huduma za moja kwa moja na uwezeshaji
zinategemea vyanzo ya nje (donors) na hivyo kukosa uendelevu pindi miradi au
programu zinapofika mwisho pia kutoweza kutekelezwa pale wafadhili
watakaposhindwa kutoa pesa kwa wakati kutokana na ucheleweshwaji au hali ya
kiuchumi kwenye nchi wahisani.
Kwa uzoefu na
changamoto hizo, Shirika la Door of Hope to Women and Youth Tanzania (DHWYT)
linaendesha mpango maalumu wa “Tuwawezeshe
kwa Rasilimali Zetu” (TRZ – Program) kama mpango wake wa ukusanyaji
rasilimali, Lengo la mpango huu ni Kuhamasisha ushiriki wa watanzania wote
waliofanikiwa kuona umuhimu wa kuchangia mipango ya uwezeshaji wa makundi ya
pembezoni na hasa vijana, Wanawake, na Watoto. Mpango huu unalenga kuomba
Wasanii vijana, taasisi binafsi, taasisa za umma, viongozi wa umma, wafanyabiashara na wazalendo
kujitoa na kuchangia gharama za miradi ya kijamii inayolenga kuwasaidia vijana
na wanawake kwenye Nyanja za kiuchumi, afya, elimu ya uraia, na ushiriki wa
vijana kwenye masuala ya umma.
Katika kufanikisha
utelekezaji wa programu DHWYT inatekeleza mpango wa TRZ wenye lengo la
Kuhamasisha na kukusanya rasilimali fedha na vitu kutoka kwa wadau wa maendeleo
wa ndani ya nchi wakiwemo Makampuni, Wasanii na Watu binafsi waliofanikiwa ili
kuweza kufanikisha ufikiwaji wa vijana na wanawake wa pembezoni na vijijini.
MALENGO
MAHUSUSI
1. Kupunguza utegemezi wa wahisani wa
nje ya nchi
2. Kuongeza ushiriki wa watanzania
wazalendo hasa vijana kuona umuhimu wa uwezeshaji wa watanzania wenzao kwa
rasilimali zetu wenyewe.
3. Kufanikisha upatikanaji wa
rasilimali kwa asilimia 100 na kuchangia uelewa wa wananchi kwenye kue
ndeleza na kusimamia miradi ya maendeleo
4. Kutoa nafasi kwa serikali, kuona namna inavyoweza kuwa na kikapu cha pamoja cha wadau kuchagia maendeleo ya ndani kama zilivyo nchi nyingine zilizoendelea